
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Mohammed Ali Kawaida, amesema amesikitishwa na kile alichodai ni matamshi ya Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa, kuhusu ushiriki wa waumini wa Kanisa Katoliki katika masuala ya kisiasa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga, Septemba 29, 2025, Kawaida amesema alitarajia kauli ya kiongozi huyo wa dini iwe ni sauti ya mshikamano katika jamii, badala ya maneno ambayo amedai yanaashiria mgawanyiko.
“Nimesikitishwa sana na matamshi yake ambayo sasa nyote mnayafahamu, na nisingependa kuyarudia hapa. Yamenisikitisha sana,” alisema Kawaida.
Ameongeza kuwa walichotarajia ni kuona sauti ya mshikamano kutoka kwa Rais wa TEC, lakini badala yake amedai wameona sauti ya “kutenga watu, kusahau ukweli na kujenga roho isiyo na mshikamano,” jambo alilosema halina nafasi katika taifa.
Hata hivyo, katika tukio alilolirejelea Kawaida, yaani Septemba 25, 2025, wakati wa Misa Takatifu ya Kilele cha Jubilee ya miaka 100 ya Seminari Kuu ya Mt. Paulo Mtume Kipalala Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, Rais wa TEC, Askofu Pisa, alieleza kuwa kwa mujibu wa sheria za Kanisa Katoliki, viongozi wa Kanisa wakiwemo Mapadri na Watawa hawaruhusiwi kushiriki katika kampeni zozote za kisiasa.
Aidha alisema viongozi hao hawapaswi kutambulishwa na chama chochote wala kuvalishwa vazi lolote la chama chochote cha siasa.