Wed. Nov 5th, 2025

Klabu ya Yanga SC imefanikiwa kukamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji mahiri Feisal Salum maarufu kama Fei Toto, kutoka Azam FC, na kumrejesha rasmi Jangwani kwa kandarasi ya miaka miwili hadi mwaka 2027, ikiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi.

Usajili huu mkubwa umetangazwa leo na kuthibitishwa na pande zote mbili, ambapo Yanga SC kupitia mitandao yao ya kijamii walituma ujumbe mfupi lakini mzito,Done Deal,FEITOTO is Green & Yellow again, ishara ya mapokezi ya mchezaji wao wa zamani ambaye alikuwa kipenzi cha mashabiki.

Fei Toto, ambaye aliwahi kuichezea Yanga SC kabla ya kujiunga na Azam FC mwaka 2022, anarudi akiwa na uzoefu mkubwa zaidi na kiwango kilichoimarika, huku akitajwa kuwa miongoni mwa viungo bora zaidi wa kati na washambuliaji nchini.

Katika misimu miwili aliyotumikia Azam FC, Fei Toto ameonesha kiwango cha juu cha ubunifu, uelewa wa mchezo, pasi zenye macho na mabao muhimu – mambo yaliyomfanya aendelee kuvutia vilabu vikubwa vya ndani na nje ya nchi.

Akizungumza kwa kifupi baada ya usajili wake kuthibitishwa, Fei Toto alisema.

Nimerudi nyumbani, Yanga ni sehemu ya moyo wangu. Nipo tayari kupambana kwa ajili ya jezi hii na kuhakikisha tunapata mafanikio zaidi.

Kwa upande wake, viongozi wa Yanga SC wameeleza kuridhishwa kwao na kurejea kwa mchezaji huyo, wakisema kuwa ni sehemu ya mpango wao wa kujenga kikosi imara kuelekea michuano ya kimataifa na kutetea mataji ya ndani.

Mashabiki wa Yanga SC wamelipokea taarifa hii kwa furaha kubwa, huku mitandao ya kijamii ikifurika na picha, video na jumbe za kumkaribisha Fei Toto nyumbani.

Wengi wanamwona kama kiungo wa mabadiliko ambaye ataziba pengo lililoonekana baada ya msimu uliopita kukamilika.

Kwa sasa, macho yote yataelekezwa kwenye mazoezi ya kikosi cha Yanga SC kuelekea msimu mpya, huku Fei Toto akiwa kivutio kikuu kwenye kikosi hicho kipya cha ndoto.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *