Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ametoa tamko rasmi kufuatia hatua ya Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kuufungia Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa kutotumika katika michezo ya fainali ya mashindano ya kimataifa. Tamko hilo limetolewa kufuatia sintofahamu iliyozuka miongoni mwa wadau wa michezo na wananchi, hususan mashabiki wa soka nchini.
Katika kauli yake, Majaliwa alisema kuwa Serikali kupitia mamlaka husika imekagua Uwanja wa Benjamin Mkapa na kubaini kuwa uko katika hali nzuri na tayari kwa kuchezewa mechi yoyote, hata kama ingefanyika leo. Alibainisha kuwa matengenezo na maboresho mbalimbali yamefanyika uwanjani hapo, ikiwemo nyasi, vyumba vya kubadilishia nguo, taa za uwanjani, pamoja na sehemu za waandishi wa habari.
“Tumefanya ukaguzi wa kina, na tunaweza kusema kwa uhakika kuwa Uwanja wa Benjamin Mkapa uko tayari. Kama kuna mechi ya fainali leo, inaweza kuchezwa hapa bila wasiwasi,” alisema Waziri Mkuu.
Hata hivyo, licha ya msimamo huo wa Serikali, Majaliwa alisisitiza kuwa hawana nia ya kuingilia maamuzi ya CAF wala Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Alisema kuwa taasisi hizo zina mamlaka kamili ya kufanya maamuzi yao kwa mujibu wa taratibu na kanuni za kimataifa. Alisisitiza umuhimu wa kuheshimu taasisi na kushirikiana kwa mazungumzo ya kiungwana ili kuhakikisha maslahi ya taifa yanazingatiwa.
“Hatuna lengo la kuingilia CAF wala TFF. Tunaheshimu maamuzi yao, lakini ni muhimu kueleza ukweli kwamba uwanja wetu uko tayari. Tupo tayari kwa majadiliano yoyote kwa maslahi ya michezo nchini,” aliongeza.
Hatua ya CAF kuufungia uwanja huo imekuja wakati klabu ya Yanga SC ikiwa inajiandaa kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF, hali iliyozua maswali mengi juu ya maandalizi ya miundombinu ya michezo nchini. Waziri Mkuu alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika viwanja vya michezo na kuhakikisha Tanzania inakuwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya kimataifa kwa mafanikio.
Tamko hilo la Waziri Mkuu limepokelewa kwa hisia tofauti miongoni mwa wadau wa michezo, ambapo wengi wanapongeza juhudi za Serikali kuhakikisha viwanja vinaboreshwa, huku wakitoa wito kwa vyombo vya michezo kushirikiana kwa karibu zaidi kwa ajili ya maendeleo ya soka la Tanzania. Je Maoni yako ni yapii wewe Kama mwanaspoti tukutane kwa komenti…..?