Yanga na Zamalek Vita Nzito Kumpata Kocha Rhulani Mokwena
Yanga SC inaendelea kupasua kichwa juu ya kocha gani imchukue kwa ajili ya kulijenga upya benchi la ufundi la msimu ujao, na sasa ni kwamba kuna uwezekano mkubwa ikapoteza chaguo jingine la tatu kwenye mawindo hayo.
Hesabu za Yanga SC zilikuwa kwa makocha watatu bora, ilianza na Marcel Koller aliyekuwa Al Ahly ya Misri lakini inaelezwa jamaa alichomoa akitaka kupumzika huku akiwa na ofa kubwa kutoka Asia.
Nje ya Koller Yanga SC ikamrukia Jose Riveiro aliyekuwa kocha wa Orlando Pirates ya Afrika Kusini aliyechukuliwa fasta na Al Ahly ya Misri aliyeenda kuziba nafasi ya Koller kwa wababe hao.
Kumbuka msimu huu Ahly ilikuwa kundi moja na
Orlando katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Mreno huyo alivuna pointi ane mbele ya timu hiyo kutoka Misri.
Baada ya hapo Yanga SC ikatua kwa Rhulani Mokwena aliyewahi kuzinoa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Wydad Casablanca ya Morocco waliotemana hivi karibuni, ambaye kwa mujibu wa mabosi wa Yanga SC mazungumzo yalikuwa yanakwenda vizuri lakini wiki iliyopita mambo yakabadilika kutokana na masharti aliyoyatoa kocha huyo raia wa Afrika Kusini.
Hata hivyo, Yanga SC imezipata taarifa kuwa Mokwena anafanya mazungumzo pia na Zamalek ya Misri huku akiwapa masharti kuwa mshambuliaji wa Jangwani, Clement Mzize anataka uwe usajili wake wa kwanza.