BAADA ya kuikanda Simba kwa mabao 3-1 katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), Meneja wa Singida Black Stars aliyewahi kuitumikia timu hiyo miaka ya nyuma, Amissi Tambwe amesema haoni kitakachoizuia msimu huu kuandika historia ya kubeba ubingwa wa michuano hiyo.
Ushindi huo uliopatikana wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, uliopo mjini Babati Manyara, umeifanya Singida kutinga fainali ya kwanza ya michuano hiyo na sasa itavaana na Yanga katika mechi ya fainali itakayopigwa kati ya Juni 26-28.
Akizungumza na Mwanaspoti, Tambwe alisema anaiona Singida BS ikinyanyua kwapa msimu huu kwa kutwaa kombe hilo dhidi ya Yanga kutokana na ubora wa kikosi walichonacho ambacho kina uchu wa mafanikio.
“Ndio tunaanza kukusanya mataji sasa, msimu huu hatumalizi bila kikombe hatua tuliyofika ya kucheza fainali hatujabahatisha ni kutokana na ubora wa timu kama tumeifunga Simba kwa idadi kubwa ya mabao tuna nafasi ya kufanya hivyo hata katika fainali,” alisema Tambwe aliyewahi kuitumikia Simba 2013-2014 kisha kuachwa na kutua Yanga na baadae kwenda Oman na Djibouti.
“Uwezo huo upo Singida Black Stars ina timu nzuri na bora ukiondoa kuangalia uwezo wa mchezaji mmoja mmoja wapo vizuri pia kwa ujumla, naamini hili linawezekana ni suala la muda tu mipango inaendelea kusukwa na wachezaji wanalitaka taji,” aliongeza Tambwe aliyewahi kuitumikia pia Singida Big Stars akiipandisha Ligi Kuu ikitumia jina la DTB kisha kuwa SBS kabla ya kubadilishwa jina na kuwa Singida Fountain Gate (sasa Fountain Gate).
Tambwe alisema anaiheshimu Yanga, lakini ana imani kubwa Singida itashinda mechi hiyo ya fainali.
Akizungumzia ligi kwa ujumla alisema, inazidi kuwa bora msimu hadi msimu na anafurahishwa na namna wachezaji wa timu tofauti wanavyoonyesha ushindani mkubwa dhidi ya timu kongwe za Simba na Yanga huku akisema SBS itatisha.