Dk. Hussein Ali Mwinyi, kuizawadia Simba SC Sh279 milioni endapo itafanikiwa kutwaa ubingwa CAFCC

Rais Mwinyi pamoja na wachezaji wa simba sports club
Rais Mwinyi pamoja na wachezaji wa simba sports club

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuizawadia Klabu ya Simba, Dola za Marekani 100, 000 (Sh279 milioni) endapo itafanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Mechi ya Simba dhidi ya Berkane ya Morocco inatarajiwa kuchezwa kesho Jumapili saa 10: 00 jioni katika uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar.

Katika mechi hiyo ambayo Rais Mwinyi atakuwa mgeni rasmi, pia amelipia gharama za uwanja ambazo ni asilimia 15 ambazo zilitakiwa kulipwa na Simba.

Dk. Mwinyi ametoa ahadi ya kiasi hicho alipokutana na kuzungumza na viongozi pamoja na wachezaji wa klabu ya Simba katika Hoteli ya Madinat Al Bahr jioni hii Mei 24, 2025.

Pamoja na ahadi hiyo, kiongozi huyo wa nchi amewatia moyo wachezaji na kuwatakia kila la heri kuelekea mchezo wao wa fainali.

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) zinaunga mkono juhudi za klabu ya Simba zilizowezesha kufikia hatua ya fainali,” amesema

Amewahimiza wachezaji kucheza kwa kujiamini ili kutwaa kombe hilo kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.

Pia Dk. Mwinyi amewasihi mashabiki wa soka kuiunga mkono Simba kwa moyo mmoja na kuishangilia kikamilifu ili kuwapa hamasa wachezaji katika kutimiza ndoto ya kutwaa kombe la Shirikisho.

Leave a Comment

Comments

No comments yet. Why don’t you start the discussion?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *