MO Dewji Azuia Jaribio la Fadlu, Matola Kuondoka Simba
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohamed ‘Mo’ Dewji, amezima jaribio la Kocha Mkuu wa Klabu hiyo, Fadlu Davids, kuchukuliwa na klabu yake ya zamani, Raja Casablaca ya Morocco, pamoja na Msaidizi wake, Selemani Matola, kutwaliwa na Prisons kwa kuwaongeza mkataba baada ya kuridhishwa na mafanikio ya msimu huu.
Aidha, klabu hiyo pia inatarajia kusajili wachezaji wapya wanne, watatu wageni na mmoja mzawa, wote wakiwa ni wa daraja la juu kwenye ngazi ya kimataifa.
Habari kutoka ndani ya Klabu ya Simba zinasema kuwa, Mo amekuwa na mazungumzo na makocha hao na kukubali kuwaongeza mkataba kila mmoja kutokana na kile ambacho wamekifanya kwenye mechi za Ligi Kuu pamoja na kimataifa.
Chanzo chetu kimesema licha ya Simba kulikosa Kombe la Shirikisho pamoja na FA, lakini bilionea huyo amekunwa na mafanikio ya muda mfupi tu yaliyoonekana licha ya kuwa na wachezaji wengi wapya, ambao ni mara ya kwanza si kuichezea Simba, bali hata mechi za kimataifa za ngazi ya kombe hilo.
“Fadlu na Matola wote wanamaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu huu, Raja Casablaca tayari ilikuwa imeshaongea naye, ilitaka kumrudisha nyumbani ili awe kocha mkuu, Matola naye Prisons ilishaanza kuongea naye ili aende kuwa kocha wao, lakini mazungumzo yao na Mo, yamevunja kila kitu, sasa watasalia Simba na amewahakikishia kufanya usajili mkubwa, mzuri wa maana ili kikosi kizidi kutisha msimu ujao,” alisema mtoa taarifa wetu.
Chanzo hicho kimesema Simba inatarajia kutenga kiasi cha Sh. bilioni tano hadi sita, kwa ajili ya kusajili wachezaji wao wanne ambao viwango vyao ni vya kimataifa.
“Wachezaji watakaosajiliwa msimu ujao ni wa daraja A, ambapo ripoti za mwalimu ambazo ameshaanza kuwaambia mabosi wake ni kupata straika wa kati mwenye uwezo wa juu wa kucheka na nyavu, msaidizi wa straika ambaye ni namba 10, beki mmoja wa kati, mrefu na mwenye nguvu, pamoja na kiungo mkabaji anayeweza kucheza kuwalinda mabeki mwenye matumizi sahihi ya mguu wa kulia,” alisema mtoa taarifa huyo.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba Ahmed Ally, juzi, alibainisha kuwa wanakwenda kuboresha kikosi, wakiingiza wachezaji wachache tu kwenye nafasi zenye uhitaji kwa ajili ya msimu ujao.
Alisema kikosi cha Simba bado ni imara, lakini watakwenda kufanya maboresho kidogo.
Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu, amekiri kuwa pamoja na kwamba msimu huu walikuwa wanatengeneza timu, lakini wamevuka malengo, ingawa bado kuna mapungufu kadhaa kwenye kikosi chao.
“Mapungufu tunayaona, tulitoka kwenye kutengeneza timu, lakini ushindi tuliokuwa tunaupata tukaona kumbe tunaweza kuwa washindani na kweli tukageuka kuwa washindani, lakini haiondoi ukweli yapo na tutayafanyia kazi,” alisema.