WAKATI kikosi cha RS Berkane kutoka Morocco kikijipanga kuivaa Simba SC katika fainali ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika, hali ya hewa ya Zanzibar inaonekana kuwatesa Waarabu hao. Kwa siku kadhaa tangu kuwasili kwao Zanzibar usiku wa Alhamisi wiki hii, hali ya hewa inayofikia nyuzi joto zaidi ya 32°C mchana imekuwa kero kwa kikosi hicho kutoka Kaskazini mwa Afrika ambako hali ya hewa ni baridi zaidi katika kipindi hiki cha mwaka.
.
Wachezaji wa RS Berkane wamekuwa wakionekana wakilazimika kutumia muda mwingi kunywa maji mara kwa mara hata mazoezini, jambo linaloashiria kutozoea mazingira ya Zanzibar ambayo Simba tayari imeyatumia kama kambi ya maandalizi kwa zaidi ya siku tatu sasa tangu ilipowasili.
.
Akizungumza mmoja wa viongozi wa RS Berkane, alisema: “Tunakutana na changamoto ya hali ya hewa. Joto ni kali kuliko tulivyotarajia. Hili linaathiri utimamu wa wachezaji wetu, hasa kwenye mazoezi ya mwisho. Lakini tutapambana hadi mwisho.”
.
Kwa Simba, hii inaonekana kuwa faida ya wazi, katika mechi ambayo Wekundu wa Msimbazi wanahitaji ushindi wa zaidi ya mabao mawili ili kutwaa ubingwa huo wa CAF.
Posted inCAF Confederation Cup
Joto Zanzibar laitesa Berkane
