Edo Kumwembe: Pyramids Wametuonesha Ukiwa na Pesa Unapata Mafanikio
Rafiki yetu Fiston Mayele na timu yake ya Pyramids wametwaa kombe ambalo kwetu linabaki kuwa ndoto. Ligi ya Mabingwa Afrika. Imenifikirisha. Hawa jamaa walianzishwa 2008 tu wakitumia jina la Al Assiouty. Walikuwa na makazi yao katika manispaa ndogo ya Ben Suef
.
Mwaka 2018 ikanunuliwa na tajiri kutoka Saudi Arabia, Turki Al Sheikh. Na hapo ndipo ilipobadilishwa jina kuitwa Pyramids ikahamishiwa Cairo. Sheikh aliiuza kwenda kwa tajiri mwingine, Salem Al Shamsi. Kuanzia kwa Sheikh hadi tajiri wa leo Pyramids wamezoea kutia pesa pale inapohitajika.
Matokeo yake msimu huu wametwaa ubingwa wa Afrika. Hii maana yake nini? Maana yake rafiki zetu wametwaa ubingwa mbele ya wale watani wa Kariakoo, Simba na Yanga. Hawa watani mmoja alianzishwa 1935 mwingine akaanzishwa 1936.
Pyramids wametuonyesha kwamba ukitia pesa unapata mafanikio. Bahati nzuri sisi wenyewe ni mfano mzuri wa matumizi ya pesa za Pyramids. Walimtaka Fiston Kalala Mayele akiwa wa moto pale Yanga na amewapa ubingwa.
Bahati mbaya kwetu ni kwamba wakati wao wakitia pesa, sisi tunaonekana kuwa klabu ambazo bado kazi yake ni kulisha wenye pesa zao. Mayele ni mfano mwingine tu, lakini wakati fulani TP Mazembe wakiwa na matumizi makubwa ya pesa walitia pesa pale Simba na kuondoka na Mbwana Samatta ambaye alienda kuwapa ubingwa wa Afrika.
Ndivyo ilivyo. Samaki mkubwa anamla samaki mdogo. Safari hii Wydad Casablanca wameondoka na Stephane Aziz Ki. Utashangaa nini kama Aziz KI akiungana na mafundi wenzake kule Morocco na akatwaa ubingwa wa Afrika? Hauwezi kushangaa sana.
.
Matokeo yake tumebaki kushangilia kufika fainali za Shirikisho mara mbili katika miaka ya karibuni. Sio mbaya, lakini safari bado ni ndefu. Kama robo huwa ni mwisho katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, basi tunahitaji tuendelee kutia pesa tena na tena.”
— Legend, Edo Kumwembe. [via Mwanaspoti