YANGA inaendelea na mkakati wa kuuza mastaa na sasa staa mwingine ambaye anapasua vichwa vya mabosi ni kipa Djigui Diarra.
Taarifa za Diarra ni kwamba ana hesabu za kutaka kuachana na klabu hiyo akishinikiza imuuze, lakini maombi yake yamewagawa mabosi wa juu.
Diarra bado ana mkataba na Yanga akiwa anaendelea kumfukuza kwa karibu kipa wa Simba, Moussa Camara katika ‘clean sheet’ za Ligi Kuu Bara wakitofautiana moja Camara akiwa na 16 na Diarra 15 huku timu wanazochezea zikichuana katika mbio za ubingwa.
Kuna makundi mawili yameibuka ndani ya Yanga hasa mabosi ambapo lile la kwanza linadai kipa huyo anayeitumikia kwa msimu wa nne tangu alipotua Agosti 2021 akitokea Stade Malien ya Mali aruhusiwe kuondoka ikipatikana timu ya kumnunua kwa fedha ndefu.
Kundi hilo la kwanza linaamini kipa huyo ni kama anaendelea kushuka taratibu akiwa kama anapoteza morali ya kufanya kazi kwa nguvu. “Hawa wanaona kama Diarra alipoteza tuzo msimu uliopita, lakini hata msimu huu hakuanza sawasawa, labda huku mwishoni ndio ameamka,” alisema bosi mmoja ndani ya timu hiyo.
Kundi la pili ni lile linalopata wasiwasi kama endapo kipa huyo ataondoka watakuwa na mbadala wa maana wa kuziba nafasi yake. “Wengine tunaona wasiwasi kwa kuwa bado hatuonyeshwi mtu muafaka ambaye kama tutamruhusu Diarra kuondoka nani atachukua nafasi yake na tukasema kweli huyu ni mtu muafaka kwa hiyo bado hatujapata muafaka.”
Posted inTetesi za Usajili
Diarra awagawa mabosi Yanga
