Pengine taarifa hii itawashusha presha mashabiki wa Yanga SC, wanaoianza wiki ya kwanza ndani ya Juni, baada ya kubainika kuwa, lile dili la kipa namba moja wa timu hiyo, Djigui Diarra anayetakiwa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini limeota mbawa baada ya kuondolewa rasmi katika hesabu za mabosi.
Iko hivi. Kaizer Chiefs ilikuwa na hesabu za kumsajili Diarra baada ya makocha wa timu hiyo wakiongoza na Nasreddine Nabi kuhitaji kipa mpya wa boli ili timu hiyo ianze kutengeneza mashambulizi kuanzia nyuma.
Katika mapendekezo ya benchi hilo la ufundi, jina la Diarra lilikuwamo akibebwa na kumbukumbu ya kufanya kazi na Nabi aliyemsajili Yanga wakati akiifundisha timu hiyo na kufika nao fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ilipopoteza kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria.
Hata hivyo, taarifa za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo ni kwamba mabosi wa Kaizer wameliondoa jina la Diarra baada ya kupata uhakika wa muda uliosalia wa mkataba alionao na Wanajangwani.
Credit × Mwanaspoti