Timu ya Nigeria Yatinga Hatua ya 16 Bora AFCON, Tunisia Kuamua Hatma ya Tanzania

Timu ya Taifa ya Nigeria imefanikiwa kutinga hatua ya 16 Bora ya michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Tunisia katika mchezo uliochezwa leo nchini Morocco.
Nigeria, inayoshiriki Kundi C, ilipata mabao yake kupitia kwa Ademola Lookman aliyefunga dakika ya 44 na 50, kabla ya Victor Osimhen kuongeza bao la tatu dakika ya 67.
Kwa upande wa Tunisia, mabao yao yalifungwa na Hannibal Mejbri dakika ya 64, huku bao la pili likifungwa na Ali Abdi dakika ya 87 kupitia mkwaju wa penalti.
Katika mchezo mwingine wa kundi hilo, Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ililazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Uganda.
Tanzania ilipata bao lake dakika ya 59 kupitia mkwaju wa penalti uliopachikwa wavuni na Simon Msuva, huku Uganda ikisawazisha dakika ya 80 kupitia Denis Omedi.
Baada ya matokeo hayo, Nigeria inaongoza Kundi C kwa pointi 6, ikifuatiwa na Tunisia yenye pointi 3, wakati Tanzania na Uganda kila moja ikiwa na pointi 1
Michezo ya mwisho ya kundi hilo itachezwa Januari 6, ambapo Tanzania itavaana na Tunisia, huku Uganda ikipimana nguvu na Nigeria.
