December 17, 2025

Taifa Stars Yapata Ushindi Mwingine Mzito Mechi ya Kirafiki

0
1765957942023.jpg

Ikiwa katika maandalizi ya mwisho kuelekea fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2024) zitakazofanyika nchini Morocco , timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imepata ushindi mzito kwa kuichapa klabu ya Arab Contractors ya Misri kwa mabao 2-0 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopigwa leo.

Katika mchezo huo uliochezwa kwa kiwango cha juu, Stars walionyesha mpango mzuri wa kiuchezaji, nidhamu ya uwanjani, na kujiamini kwa kikosi kizima – hali inayotoa matumaini makubwa kwa Watanzania kuelekea mashindano hayo makubwa barani Afrika.

Mabao ya ushindi yaliwekwa kimiani na nyota wa Stars na Azam Fc, Feisal Salum ‘Fei Toto’ pamoja na Tarryn Allarakhia, wakiihakikishia Tanzania ushindi wa kuvutia mbele ya wapinzani kutoka ligi ya juu ya Misri.

Feisal Salum, ambaye kwa sasa anavaa jezi ya Azam FC, alifungua pazia la mabao kwa mkwaju mzuri uliomshinda kipa wa Arab Contractors, huku Allarakhia akihitimisha kazi safi kwa bao la pili lililozima matumaini ya wapinzani kurejea mchezoni.

Mchezo huo umekuwa kipimo kizuri kwa benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Miguel Gamondi, ambaye anatajwa pia kuwa katika mazungumzo ya kuchukua mikoba ya ukocha ndani ya Simba SC. Kikosi kimeonekana kuwa katika hali nzuri ya kimbinu, uthabiti wa safu ya ulinzi, pamoja na ubunifu mkubwa kwenye kiungo.

Hii ni ishara kuwa maandalizi ya Stars kuelekea Morocco yanakwenda sambamba na matarajio ya wadau, huku mashabiki wakiendelea kuonesha imani kwa kikosi hicho.

Kwa sasa, Stars wanatarajiwa kuendelea na kambi ya mwisho kabla ya kuelekea rasmi kwenye fainali hizo, ambapo wamepangwa kundi gumu lakini la ushindani, na lengo kuu ni kuandika historia mpya kwa soka la Tanzania barani Afrika.

Kwa ushindi huu, Tanzania inaingia kwenye AFCON na morali ya juu – ikiwa na matumaini ya kufanya vizuri zaidi kuliko ilivyowahi kutokea hapo kabla

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *