
YANGA imeanza kwa kishindo Ligi Kuu kwa kushinda mabao 3-0 dhidi ya Pamba, lakini baada ya mchezo huo kumalizika Kocha Romain Folz alijifungia na mastaa na kuwawashia moto.
Folz alikuwa mkali kwa wachezaji wa timu hiyo hasa wale waliocheza dakika 45 za kwanza, akiwapa ukweli kwamba kila mmoja ana takiwa kujitathimini kama anatosha ndani ya kikosi hicho. Inaelezwa Folz alikuwa mkali kwa wachezaji huku akishusha mikwara mzito wa kumtupa mchezaji yoyote benchi, endapo kila akipewa nafasi atashindwa kuonyesha kiwango kizuri.
“Bila shaka nakubaliana na kila mmoja hatukucheza vizuri dakika 45 za kwanza, tulijiweka kwenye presha badala ya kuwapa presha hizo wapinzani, sio mashabiki hata mimi sikuvutiwa, nawaelewa,” alisema Folz na kuongeza;
“Kama kocha nabeba hilo kwanza baada ya hapo nakwenda kuongea na timu nzima, unapokuwa mchezaji wa klabu kama hii unatakiwa kuwa tayari kufanya kikubwa kwa uzito wa jezi ya timu hii.
Hatukuwa na chaguo lingine zaidi ya kubadilisha kikosi ili kulinda viwango vya wachezaji, ratiba yetu ngumu sana, kuna wakati tunatakiwa kufanya rotesheni kubwa ili kulinda afya pia za wachezaji.