Licha ya kutimiza ndoto yake ya kucheza Barcelona, lakini mpango uliopo wa mabosi wa miamba hiyo ya Ligi Kuu Hispania, La Liga, ni kumrudisha mshambuliaji Marcus Rashford England kutokana na kutokuridhika na kiwango chake.

Rashford alitua Barca dirisha la usajili la majira ya kiangazi lililopita kwa mkopo akitokea Manchester United baada ya kushindwa kuingia kwenye kikosi cha Kocha Ruben Amorim kutokana na kutokuelewana kwa wawili hao, ikiwamo kutoendana na mfumo wake.

Ripoti iliyotolewa na vyombo vya habari vya Hispania inaeleza nyota huyu, 27, aliyekuwa na ndoto ya kucheza Nou Camp hajawaridhisha mabosi wa Barca kutokana na kiwango cha chini alichoonyesha katika mechi za mwanzo na wanajadili uwezekano wa kumsitishia mkataba wake kabla ya Krismasi.

Awali kulikuwa na kipengele kitakachoiruhusu Barca kumnunua jumla kwa Pauni 30 milioni mwisho wa msimu, lakini kutokana na kiwango duni, huenda akarudi Old Trafford licha ya kwamba miamba hiyo ya Catalonia bado italazimika kuilipa Man United Pauni 4.3 milioni kama fidia ya kuvunja makubaliano.