
KAMBI ya Yanga inayojiandaa na msimu mpya wa mashindano kwa mwaka 2025-26, imezidi kunoga kwa kocha Romain Folz kuendelea kuwapika mastaa wa timu hiyo, huku akikomalia mechi za kirafiki kujenga utimamu wa wachezaji wake, lakini nyota wa kikosi hicho Prince Dube amevunja ukimya na kuzungumzia vita ya namba kutokana na ongezeko la wachezaji wapya.
Dube amekiri ongezeko la wachezaji wapya katika eneo la ushambuliaji analotumika yeye kwa sasa limeongeza ushindani, licha ya kutamba kuwa hana presha, isipokuwa kunamuongezea ubora zaidi.
Hadi sasa Yanga imeshacheza mechi mbili za kirafiki tangu ilipotoka Rwanda kucheza na Rayon Sports na kuifunga mabao 3-1, kwa kuinyuka Fountain Gate kwa mabao 2-1, yaliyowekwa wavuni na Prince Dube na Aziz Andambwile na juzi imeifunga Tabora United 4-0, mabao yakifungwa na Pacome Zouzoua, Prince Dube na Celestin Ecua aliyetupia mbili.
Dube ambaye msimu uliopita alifunga mabao 13 ya Ligi Kuu akiwa nyuma ya Clement Mzize aliyefunga 14, hadi sasa katika mechi za kutesti mitambo akiwa ameshatupia mawili, aliliambia Mwanaspoti, hana presha juu ya ujio wa wachezaji wapya katika eneo analocheza na badala yake anafanya kazi yake kwa kuhakikisha anaonyesha uzoefu wa ligi na uwezo alionao.
Mshambuliaji huyo aliyesajiliwa na Yanga akitokea Azam FC, akiwa tayari ametwaa mataji matano msimu uliopita, alisema ujio wa washambuliaji ni faida kwa klabu na imeongeza ushindani mkubwa, lakini kwake pia kwani anapambana kuhakikisha anafanya kilicho bora zaidi msimu ujao.
“Kuongezewa changamoto inaweza kukujenga na kukuangusha pia lakini naweza kusema nimeshakuwa mkomavu kwenye mpira, siwezi kuwa na presha, zaidi napambana kuonyesha uwezo ili kujihakikishia nafasi niliyonayo ndani ya timu,” alisema straika huyo raia wa Zimbabwe aliyeongeza;
“Nimeangalia usajili uliofanywa, kuna wachezaji wazuri na wenye uwezo mkubwa. Ni nafasi yangu kuendelea nilipoishia kwa kuipambania timu na mimi binafsi sio rahisi kutokana na uwepo wa kocha mpya, mchezaji yeyote anaweza kupata namba kulingana na namna atakavyoonyesha kwenye uwanja wa mazoezi.”