WATETEZI wa michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za ndani (CHAN), Senegal imeanza vizuri kampeni za kutetea taji hilo baada ya kuifunga Nigeria ‘Super Eagles’, bao 1-0, katika pambano nzuri na la kuvutia baina ya miamba hiyo.
Pambano hilo la kundi D, lililopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, lilishuhudia timu zote zikicheza soka la kushambuliana kwa dakika zote 90, ingawa ilikuwa Senegal iliyoibuka na ushindi.
Katika mechi hiyo iliyokuwa ya vuta nikuvute kwa timu zote mbili, iliichukua Senegal kupata bao la ushindi dakika ya 75, lililofungwa na nyota wa kikosi hicho, Christian Gomis, baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Nigeria.
Simba wa Teranga’, inashiriki michuano hii kwa mara ya tatu baada ya kufanya hivyo mwaka 2011 na 2022, ilipotwaa taji hilo katika fainali ilipowafunga wenyeji, Algeria kwa mikwaju ya penalti 5-4, kufuatia miamba hiyo kutoka suluhu (0-0) dakika 120.
Kikosi hicho kinachoshika nafasi ya 18 katika viwango vya ubora wa FIFA, huku kikiwa kinafundishwa na Kocha, Souleymane Diallo, kilipata tiketi ya kushiriki michuano ya CHAN 2024, baada ya kuitoa timu ya Taifa ya Liberia kwa jumla ya mabao 4-1.
Kwa upande wa Nigeria, inashiriki michuano ya CHAN kwa mara ya nne kuanzia 2014, 2016, 2018 na 2024, huku ikiwa na benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Daniel Ogunmodede.
Kikosi hicho kilichoonyesha soka safi leo dhidi ya Senegal licha ya kupoteza, kilikata tiketi ya kushiriki michuano ya CHAN 2024 baada ya kuitoa Ghana kwa jumla ya mabao 3-1.
