FAINALI za CHAN zinatarajiwa kuanza Agosti 2 na Tanzania πΉπΏ Kenya π°πͺ na Uganda πΊπ¬ zinaandaa kwa pamoja ikiwa ni kwa mara ya kwanza kwa mataifa hayo.
Michuano hii inafuatiliwa na mataifa mengi ndani na nje ya Afrika na hivyo ni wazi wachezaji watapata nafasi ya kuonekana huko kutokana na ushiriki wao katika tiumu za taifa. Hii ni wazi hata wanaosaka vipaji kwa maana ya skauti na mawakala kutoka timu mbalimbali kubwa za Afrika na hata nje ya Afrika watamiminika kuangalia nyota watakaokiwasha na kuwachukua kwa ajili ya kuwapeleka timu kubwa.
Hii ni fursa kubwa wa wachezaji wa Stars watakaokuwa katika kikosi cha Stars na wanatakiwa kujua wanapocheza mbali na mashabiki kushuhudia vipaji vyao watakuwa wanatazamwa na mawakala na hivyo kazi ni kwao kujitahidi kuonyesha uwezo. Ni wazi hata klabu za Tanzania zinasubiri michuano hii ili kusaka wachezaji watakaowasajili dirisha hili, hivyo, hata wa Stars watakuwa wakitazamwa.
Kuonyesha kipaji haimaanishi wachezaji wawe wabinafsi uwanjani, bali hata kucheza kitimu na muunganiko wao ni moja ya sababu zinazoangaliwa kwa mchezaji. Pia vipo vigezo mbalimbali vinavyowafanya mawakala kusaka nyota wa kuwapeleka timu kubwa ikiwamo nidhamu na kujituma na katika hili ndiyo litakalowawezesha nyota wa Stars kutimiza ndoto zao za kucheza nje ya nchi.
Tunaamini hata nyota wa Stars wanalijua hilo na watapambana kuiwakilisha vyema nchi huku pia wakiuza vipaji vyao. Soka ni biashara kubwa kwa sasa na wachezaji wanauzwa kila kona ya dunia kwa pesa nyingi ambazo wengi zinabadilisha maisha yao. Mifano ni mingi kwa nyota waliofanikiwa kutokana na soka licha ya kuwa walikuwa na maisha duni katika familia zao.
Nyota wengi Amerika ya Kusini wametokea maisha duni na kutokana na soka wamejikuta wakitoboa kimaisha na sasa wanaogelea kwenye ukwasi na kusaidia familia zao na jamii.
Soka ni kazi kama nyingine na yenye kipato kizuri endapo mchezaji atajituma na kuwa na nidhamu na si kubweteka baada ya kusajiliwa na kulipwa fungu la kwanza la usajili. Michuano hii ya Chan ni fursa pekee ikiwa dirisha la usajili pia bado liko wazi hadi hadi itakapomalizika Agosti 30.
