Mashabiki wa Simba SC wameibuka na mjadala mzito mitandaoni wakimshutumu beki wao, Hamza, kwa kile wanachokiita kuwa ni “muoga wa mechi kubwa” na kwamba ana tabia ya kujiondoa kwenye michezo yenye presha kubwa kwa kudai majeraha.
Katika mchezo wa kwanza wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane uliopigwa mjini Morocco, Hamza alipewa nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza. Hata hivyo, katika dakika za pili za kipindi cha pili, alionekana kushindwa kuhimili kasi ya wapinzani na hatimaye alihusika moja kwa moja katika kosa lililosababisha goli la pili la Berkane. Baada ya tukio hilo, alionekana kuomba kutolewa akidai kuumia.
Kitendo hicho kimezua mijadala mikali mitandaoni huku baadhi ya mashabiki wakikumbusha matukio ya nyuma, wakidai kuwa Hamza alifanya hivyo pia kwenye mechi ya watani wa jadi dhidi ya Yanga SC na ile dhidi ya CS Constantine, ambapo hakuweza kuendelea na mashindano kwa madai ya majeraha dakika chache kabla ya mechi hizo.
“Watu wanaanza kumlinganisha na mabeki kama Dickson Job au Bacca, lakini ukweli Hamza bado hana uthubutu wa kupambana kwenye mechi za presha. Kuna wakati anatabia ya kujivunja ili asiendelee na mchezo,” aliandika shabiki mmoja kwenye mtandao wa X.
Ingawa wapo mashabiki wanaomtetea wakidai ni mchezaji mwenye uwezo mzuri kiufundi, bado lawama hizi zinaonyesha kuwa Hamza anahitaji kujitathmini na kujiimarisha zaidi kisaikolojia kwenye mechi kubwa.
Je, atajibu shutuma hizi kwa matendo kwenye mechi ya marudiano itakayopigwa jijini Dar es Salaam? Wakati ndio utatoa majibu.